Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuwa alitoa tamko alipokuwa jimboni kwake kukataza shughuli na mikutano ya vyama vya siasa kwa kuwa sasa ni muda wa kazi tu.

Akijibu swali lilioulizwa na kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu mapema leo asubuhi, alisema kuwa mwandishi wa habari hiyo hakufuatilia kauli yake vizuri na kuoanisha na mazingira husika.

Alisema kuwa alipokuwa jimboni kwake  alizungumza kama Mbunge wa Ruangwa kwa ajili ya Ruangwa na kukubaliana na madiwani wa jimbo hili wakiwemo wale wa upinzani, na ilihusu jimbo hilo.

“Jambo lile lilitokana na mazingira ninayoishi na nililitamka kama mbunge, sikulitamka kama Waziri Mkuu na lilitokana na matamko ya sisi wanasiasa tulioko katika jimbo lile.

Alisema kuwa yeye pamoja na madiwani wa CCM na wa upinzani, walikubaliana katika kuungana na kuweka pembeni siasa pamoja na itikadi zao na kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi.

“Kama mwandishi angeandika vizuri kwa kueleza shughuli zangu… hata nilipotamka kwamba ‘kuanzia sasa sisi tumeamua tufanye kazi tu bila kuzingatia itikadi ya vyama vyetu. Na kwamba sasa mambo ya siasa tuache pembeni. Wale wote ambao sasa wanatakiwa kupita katika maeneo ya walioshinda, ni wale tu walioshinda kwenye maeneo yao,” alisema Waziri Mkuu.

Alifafanua kuwa yeye ni muumini wa demokrasia na hawezi kuzuia wanasiasa kuendelea kufanya kazi zao za kisiasa bali mwandishi wa habari ile ndiye aliyeandika bila kuzingatia  hayo aliyoeleza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alijibu kipengele cha pili cha swali la Mbowe na kueleza kuwa Serikali ilipokea mapendekezo kutoka TBC kuhusu gharama wanazoingia kwa kurusha vikao vya bunge live na kushauri njia mbadala ambazo serikali ilikubaliana nazo.

“Waziri mwenye dhamana alifafanua vizuri hapa jana, na huo ndio msimamo wa serikali,” alisema Waziri Mkuu.

 

CUF watoa Msimamo Rasmi kuhusu Ushiriki wa Marudio ya Uchaguzi Zanzibar
Bashe ameungana na Ukawa? Zitto na Mbowe warejesha ‘kicheko’