Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Taka mjini Lindi(LUWASA), Adam Alexanda kuanzia leo Oktoba 19, 2016 kutokana na kushindwa kusimamimia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi pamoja na matumizi mabaya ya ofisi. Waziri mkuu ameitaka Taassisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa(TAKUKURU) mkoani Lindi kumhoji Mkurugenzi huyo.

 

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 19, 2016 wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ng’apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.

“Kamanda wa TAKUKURU fanya mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa Wizarani, mimi najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” – Waziri Mkuu.

Mkurugenzi huyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi. “Huyu nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam.”

Alipoulizwa sababu za kutokuwepo ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatulia changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.

“Unatumia siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu! Tena baada ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa sh.150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,” – Majaliwa.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake siku tatu mkoani Lindi na amerejea jijini Dar es Salaam.

 

Video: Msaada uliomfikia Waziri Mkuu kutoka kwa Mbunge Hamida

Scorpion afutiwa mashtaka na kufunguliwa upya
Mzee Akilimali: Yanga Haikodishwi Kama Masufuria Ya Shughulini