Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Mussa Msangi kwa kosa la kumdanganya kuhusu mradi wa maji aliouzindua katika kata ya Hedaru.

Amechukua uamuzi huo wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Hedaru mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Lengeni-Hedaru, wilayani Same.

Waziri Mkuu alibaini kuwepo kwa tatizo wananchi walipoanza kuzomea wakati zikitolewa salaam za utambulisho kwa viongozi alioambatana nao. Kabla hajahutubia, aliamua kumuita Mhandisi huyo aelezee ukweli wa madai ya wananchi kwamba maji yametoka kutokana na ujio wake.

“Jumuiya zote za maji nazivunja kuanzia leo, na wahusika wote watafutwe na Jeshi la Polisi. Haiwezekani nipewe kazi ya kuzindua mradi ambao hauna maji, Katibu Tawala wa Mkoa lete wakaguzi wa mahesabu kwenye huu mradi, pia leta mhandisi mwingine asimamie huu mradi. Huyu arudishwe kwa Waziri wake,” amesema Majaliwa.

Aidha, alipoulizwa kwa mwezi wanakusanya kiasi gani cha fedha kutokana na mauzo ya maji hayo, Mhandisi Msangi alijibu kwa mwaka uliopita walikusanya sh. milioni saba tu.

“Haiwezekani kama maji yanatoka, wenye kamati wapate shilingi milioni saba. Ni ama maji hayatoki au wanakusanya hela na wanazila.” amesema Waziri Mkuu.

Msiilaumu mahakama, tatizo hapa ni wapelelezi- Jaji Mkuu Prof. Juma
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 20, 2019