Operesheni ya kutumbua majipu inaendelea nchini ambapo leo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa daktari wa Hospitali ya Ligula Mkoani Mtwara, aliyedaiwa kuomba na kupokea rushwa ya shilling 100,000 ili amfanyie upasuaji mgonjwa.

Akiwa katika hospitali hiyo, Waziri Mkuu alichukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Tatu Abadallah ambaye alidai kuwa alilazimika kuuza shamba la familia ili aweze kumudu gharama za matibabu ikiwa ni pamoja na rushwa aliyoombwa na Dk. Fortunatus Namahala wa kitengo cha upasuaji.

“Februari Mosi nilimleta baba yangu hapa hospitali nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa nimnunulie dawa za shilingi 85,000 kwenye duka la hapo nje. Pia, niliambiwa ninunue uzi wa kushonea wa shilingi 25,000. Lakini Daktari naye akasema anataka shilingi 100,000 ya kwake,” Bi. Tatu alimueleza Waziri Mkuu.

Alieleza kuwa ingawa alifanikisha kumpa kiasi hicho cha fedha daktari huyo, hadi kufikia Februari 7 baba yake hakuwa amefanyiwa upasuaji kama alivyokuwa ameelezwa. Hivyo, ilimlazimu kutafuta huduma hiyo katika moja ya zahanati za watu binafsi mkoani humo.

“Tarehe 12, baba alitolewa hospitali [bila kufanyiwa upasuaji] na tukaambiwa turudi Februari 16. Niliumia kwa sababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba ilikuwa inazidi kuzorota. Ndipo baba aliniambia nirudi kijijini Kwetu Kilombero nikauze shamba la Hekari 2.5,” alieleza.

Kwa mujibu wa Tatu, alifanikiwa kuuza shamba hilo na baada ya kupata fedha, alimpeleka katika zahanati ya Sajora ambako alilipa kiasi cha shilingi 560,000 na baba yake alifanyiwa upasuaji.

Baada ya kusikia maelezo hayo, Waziri Mkuu alimuagiza Katibu Mtendaji wa Mkoa wa Mtwara kufuatilia suala hilo na kushirikiana na Takukuru kuhakikisha Daktari huyo anachukuliwa hatua za kisheria.

Mbali na mkasa huo, Waziri Mkuu alikutana na kero nyingi kutoka kwa wananchi huku hali ya huduma ya hospitali hiyo ikiwa hairidhishi.

Waziri Mkuu aliagiza madukwa yote yaliyoko nje ya hospitali hiyo kufungwa mara moja na kuanzishwa kwa dirisha la wazee na huduma za Afya ndani ya hospitali hiyo.

Polisi wamsaka Mbunge mwingine wa Chadema, ni baada ya kuwashikilia Mdee na Kubenea
Simba Wampiga Stop Hassan Isihaka