Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza uongozi wa Wizara ya Habari, utamaduni sanaa na michezo kufuatilia hatma za malipo ya kazi za wasanii na kumpatia taarifa katibu wa wizara hiyo.

Ametoa agizo hilo jana, wakati akizungumza na viongozi wa wizara hiyo na wa wizara ya maliasili na utalii pamoja na chama cha muziki wa Rhumba Tanzania (Chamuruta) ofisini kwake jijini Dodoma.

“Hivi ni kwa nini mwimbaji wa Tanzania anatunga wimbo wake, unapigwa nchi nyingine Afrika au Ulaya, unauzwa kwenye CD ndani na nje ya nchi, wanafaidi wao lakini mwanamuziki wetu hapati malipo yoyote” aliuliza Waziri mkuu.

Na kuongeza kuwa “Nimewasikia wakisema Taifa fulani mwanamuziki anafaidika hata baada ya kufariki, hivi taifa hilo wanafanya nini hadi wanafaidika na sisi tunafanya nini, hawa wanafaidika na sisi hatufaidiki”.

Pia amehoji sababu za wanamuziki wa rhumba nyimbo zao kutowekwa katika mtandao wa youtube licha ya kuwahi kuwasikia wasanii wa muziki wa kizazi kipya wakizungumzia suala la kuingiza pesa wanapoweka kazi zao katika mtandao huo.

Akijibu agizo hilo naibu waziri wa wizara hiyo, Juliana shonza amesema wizara hiyo itaangalia ni aina gani ya kozi zinatolewa na chuo kikuu cha sanaa Bagamoyo (Tasuba) kwani ziko za muda mrefu na mfupi, lakini watafanya kila jitihada kuhakikisha muziki wa rhumba haufi.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu amesema wako tayari kushirikiana na wanamuziki wa rhumba kuutangaza lakini ametaka wafanye mabadliko makubwa na wabadili mtazamo wao ili waweze kuendana na hali halisi ya soko sasa.

Kesi za matunzo ya watoto zaongezeka Tanga
Tanzania yaongoza miradi mikubwa ya ujenzi EAC