Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19) yanazidi kupungua kwa kiasi kikubwa, ambapo jiji la Dar es Salaam limebaki na jumla ya wagonjwa 13 tu walioko hospitalini.

Akizungumza leo akiwa msikitini aliposhiriki ibada ya Sikukuu ya Eid, Waziri Mkuu ameeleza jinsi takwimu za wagonjwa wa corona zilivyoendelea kushuka kwa kasi nchini, huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujilinda dhidi ya maambukizi.

Ametaja idadi ya wagonjwa waliopo hospitalini kwa kulinganisha idadi iliyokuwa imetajwa wiki iliyopita na Rais John Pombe Magufuli.

“Amana ndio eneo la kulaza wagonjwa, na kuna vitanda 190. Tarehe 17 Mheshimiwa Rais alituambia kuna wagonjwa 12, nafurahi kuwaambia taarifa ya Daktari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, asubuhi ya leo amebaki mgonjwa mmoja (1),” amesema Waziri Mkuu.

“Mloganzila, tahere 17 Mheshimiwa Rais alisema wamebaki wagonjwa sita (6), leo hii kwa taarifa ya Mganga Mkuu wa Dar es Salaam, amebaki mgonjwa mmoja (1),” ameongeza.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa katika Hospitali ya Temeke ambako Mei 17, 2020 Rais Magufuli alisema hakuna mgonjwa, hadi leo hali iko vilevile, hakukuwa na mgonjwa.

Aidha, alieleza kuwa katika hospitali binafsi zilizojitolea kuwapa matibabu wagonjwa wa corona, hali imezidi kuwa nzuri, kwani baadhi ya hospitali wagonjwa wote wameruhusiwa, na waliopo ni Agha Khan ambapo kuna wagonjwa 11 tu na kwamba kati ya hao wanne ndio wanaohitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Kibaha hadi sasa kuna wagonjwa 16 tu hospitalini, kutoka wagonjwa 22 walioripotiwa Mei 17, 2020; na Mkoa wa Dodoma katika Hospitali ya Mkonze iliyokuwa imetengwa kuna wagonjwa watatu tu kutoka wagonjwa 12 walioripotiwa wiki iliyopita.

“Tunaposema haya hatusemi ili tujisahau, bali Watanzania tumeendelea kujikinga, tuendelee kuwa na tahadhari ili tupunguze uwezekano wa kumuambukiza mwenza na wewe kuambukiza,” alisema Waziri Mkuu.

Awali, Tanzania iliripoti kuwa na visa 509 vya wagonjwa wa corona na vifo 21.

Wizara yaagiza samaki kuwekewa alama kabla ya kuuzwa nje ya nchi

Katavi: Mtuhumiwa ubakaji auawa kwa fimbo

Burundi: Matokeo ya awali ya uchaguzi kutangazwa leo
Katavi: Mtuhumiwa ubakaji auawa kwa fimbo