Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka waandishi wa habari na wadau wote wa Kiswahili kuweka mkakati wa pamoja wa kuitangaza lugha hiyo nje ya nchi.

Majaliwa, ametoa wito wakati akizungumza na wadau mbalimbali alipokuwa akifunga Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lililofanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil, Kikwajuni, Zanzibar.

Amesema, “Nitoe rai kwa waandishi wa habari kuimarisha ushirikiano na wataalamu wa Kiswahili na taasisi za Kiswahili kuhakikisha kwamba mnaweka mikakati thabiti ya kupenyeza Kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kuhusu umuhimu wa kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, Waziri Mkuu amesema, ” tufanye tafiti, BAKIZA na BAKITA tutumie vyuo vikuu kufanya tafiti na kubainisha majibu haya. Tutumie vizuri fursa ya UNESCO ya tarehe 7 Julai, kila mwaka kwa kuendesha makongamano na kubainisha suluhisho.”

Aidha, amewataka mawaziri wa Wizara za Viwanda na Biashara kutoka pande zote za Muungano wahakikishe kwamba bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya hapa nchini na zile zinazoingizwa kutoka nje, zinakuwa na maelezo ya Kiswahili, ili kuwapa fursa watumiaji wazitumie wakiwa wanafahamu vema maelekezo yaliyomo kwenye bidhaa hizo.#

Mbali na kuitangaza lugha hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amehimiza matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, kuweka mkakati wa kukibidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa na kuhakikisha kuwa maelezo ya matumizi ya bidhaa yanawekwa kwa Kiswahili.

Wanawake wenye ndoto za kugombea 2025 watakiwa kujijenga
Raia Afrika Kusini kumaliza maandamano usiku wa manane