Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua programu ya kompyuta maarufu kama JIBA App liyotengenezwa na taasisi ya kibiashara ya Jaffery International Business Association (JIBA) tawi la Tanzania, na kutaka uungwaji mkono kwa Serikali katika kuongeza wigo wa utoaji elimu ya fedha kwa vijana.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema programu hiyo itapunguza usumbufu na kuongeza ufanisi wa kufanya biashara, ambapo pia amezindua mfumo wa JIBA Sandbox ambao unalenga kuwawezesha wadau kupata mafunzo na elimu ya jinsi kufanya biashara kwa ufasaha na kujikuza kwenye biashara na soko ulimwenguni.

Amesema, “Programu hii inatarajiwa kupunguza usumbufu, kuongeza uwajibikaji na uaminifu kwenye sekta na mifumo ya biashara. Pia, itasaidia kupanua wigo wa soko la dunia kwa kuruhusu na kurahisisha biashara kufanyika mkononi kutoka mahali popote ulipo.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha programu hizo zinakuwa endelevu na zinatoa matunda yaliyokusudiwa, timu ya uongozi wa JIBA na wanachama wake waiunge mkono Serikali katika kuongeza wigo wa utoaji elimu ya fedha kwa vijana na kuwawezesha kutumia vizuri mitaji wanayoipata.

Programu hiyo ambayo lengo lake kuu ni kutengeneza fursa za biashara, itawezesha upatikanaji wa taarifa juu ya fursa za uwekezaji za ndani na nje ya nchi na hivyo kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wanachama wa JIBA ambao ni wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar bin Zubeir Mbwana alisema suala la biashara kuwa uti wa mgongo wa maisha ya mwanadamu linasisitizwa sana kwenye Quran tukufu huku akibainisha kuwa, “sehemu tisa katika mafungu 10 ya riziki yako katika biashara na ukulima na moja ya kumi iliyobaki iko katika ufugaji.”

Ushirikishwaji wazawa mradi SGR waifurahisha Serikali
Kamala Harris kutembelea Tanzania