Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa Serikali kupunguza muda wa kurushwa moja kwa moja (Live) kwa matangazo ya vikao vya bunge kupitia vituo vya runinga.

Akijibu maswali ya Watanzania waishio jijini London nchini Uingereza, Waziri Mkuu alisema kuwa uamuzi huo ulichukuliwa ili kuwawezesha wananchi kufanya kazi kama ilivyo kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’, na kuongeza nafasi zaidi ya wananchi wengi kuangalia Bunge nyakati za usiku.

Alisema kuwa Bunge la Tanzania lilikuwa Bunge pekee Afrika Mashariki na duniani kote ambalo lilikuwa linarushwa ‘Live’ kuanzia asubuhi hadi usiku. Alifafanua kuwa katika kipindi cha Bunge la bajeti ambalo huendeshwa kila siku kwa miezi mitatu, Watanzania pia wangekuwa wanaangalia ‘Live’ kwa kipindi chote cha miezi mitatu.

“Tulilazimika kujifunza kutoka kwenye mabunge mengine. Hivi hapa Uingereza mnaangalia Bunge live kila siku?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa kuwa linarushwa moja kwa moja kwa pipindi kisichozidi dakika 15 wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu pekee.

Aidha, alifafanua kuwa Bunge la Tanzania linarushwa ‘LIVE’ kila siku asubuhi wakati wa maswali ya kawaida na Alhamisi asubuhi wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu lakini mijadala yote hurekodiwa na kuhaririwa na kisha kurushwa kuanzia saa 8-9 mchana na saa 3-4 usiku kwa siku husika.

Alisema Watanzania waliokuwa wanafanya kazi na wanaopenda pia kufuatilia Bunge, walikuwa wanakosa fursa ya kuangalia Live kwakuwa walikuwa kazini, lakini hivi sasa wanaweza kufuatilia kwa sababu muda wa jioni uliopangwa wanakuwa wametoka kazini na wanaweza kuangalia wakiwa nyumbani.

Madee adai kuishi na Dogo Janja ni Kutimiza ndoto ya mpenzi wake aliyefariki
Mpinzani wa Rais Museveni apigwa rungu la 'uhaini' mahakamani