Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua rasmi upandaji wa miche ya michikichi kwenye mashamba ya wakulima mkoani Kigoma kutizimiza mkakati wa Tanzania kujitosheleza kwa uzalishaji wa mafuta ya mawese.

Amefanya uzinduzi huo jana kwa kutangaza mwanzo wa Kigoma ya mawese rasmi, kwenye gereza la Kwitanga wilaya ya Kigoma na kambi ya JKT Burombola kikosi cha 821 wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Amesema kuwa Serikali imewekeza nguvu za kutosha kutekeleza mpango huo na kwamba miaka mitano ijayo, Tanzania itakuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta ya mawese barani Afrika na duniani.

Kwa kuanza ametoa maelekezo kuwatambua wakulima wote wanaolima na wanaotaka kulima michikichi, kuwapa mbegu bure, kuweka mazingira ya wataalamu wa ugani kuwafikia wakati wote, kuratibu upatikanaji wa teknolojia na mikopo kwa wanaolima michikichi.

Sambamba na hilo Majaliwa amezitaka kambi za JKT Burombola na gereza la Kwitanga kusimamia kwa karibu mpango wa Serikali kwa utekelezaji wa kilimo cha mashamba makubwa ya michikichi na uzalishaji mkubwa wa mafuta ya mawese.

Naibu waziri wa kilimo, Omari Mgumba amesema kuwa serikali imeimarisha kituo cha utafiti wa michikichi Kihinga mkoani humo ambapo wataalamu 13 wamepelekwa wakiwemo watafiti tisa waliobobea kwenye michikichi ambao watawezesha kufikia lengo la kuzalisha miche milioni tano miaka mitatu ijayo.

Mgumba amesema kuwa lengo hilo linaenda sambamba na lengo la uzalishaji wa miche milioni 15 kila mwaka kwenye mikoa inayolima michikichi nchini hivyo kuwezesha Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta ya mawese.

Wizara yaagiza samaki kuwekewa alama kabla ya kuuzwa nje ya nchi
Frankfurt: Waumini 40 waambukizwa Corona baada ya ibada