Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua rasmi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahimiza vijana waliotimiza miaka 18 wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.

Ametoa rai hiyo wakati akizindua zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwenye uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi ya siku nne, ambapo ametumia fursa hiyo kuwasisitiza vijana na wale wanaorekebisha taarifa zao kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama hajajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ama hana kadi ya mpigakura.

Amesema kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. ambapo mesema kuwa litafanyika nchi nzima na linatarajiwa kukamilika Machi, 2020.

“Watakaohusika awamu hii ni wapigakura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale watakaotimiza miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama kata au Jimbo na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa sambamba na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki,” amesema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziasa asasi za kiraia ambazo zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura, zijiepushe na ushabiki wa kisiasa na badala yake zizingatie mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Nimeambiwa, Tume imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya Asasi za Kiraia. Rai yangu kwa asasi zilizopata vibali hivyo ni kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Niendelee kuwaasa pia kutohusisha ushabiki na mijadala ya kisiasa muda wote mtakapokuwa mkitoa elimu hiyo,” ameongeza Majaliwa.

Aidha, amesema kuwa ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, basi watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha katika daftari hilo na hatimaye kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage, amesema kuwa katika zoezi la sasa, Tume itaendelea kutumia teknolojia ya kielektroniki ya Biometric (BVR) na imeandaa BVR kits 3,000.

Amesema kuwa kwa Tanzania Bara, Tume hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji kutoka 36,549 vilivyotumika mwaka 2015 hadi kufikia 37,407; kutokana na zoezi la uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura lililoendeshwa mwaka jana.

“Kutokana na hilo, vituo 6,208 vilibadilishwa majina, vituo 817 vimehamishwa kutoka mtaa mmoja au kijiji kimoja na kwenda kingine na vituo 19 vilihamishwa kutoka kata moja kwenda kata nyingine.”

“Kwa upande wa Zanzibar, vituo vya uandikishaji vimeongezeka kutoka 380 na kufikia 407. Kwa sasa kila kijiji au mtaa, utakuwa na kituo kimoja,” amesema Kaijage.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 19, 2019
Video: Mbunge CCM aonya, 'Huyu Kinana na Makamba wasimvuruge JPM- Dkt. Chegeni