Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi ukamilishe upelelezi na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wote wanao daiwa kuhusika katika tukio la wizi wa nondo 135 za mradi wa ujenzi wa wodi ya daraja la kwanza kwenye hospitali ya wilaya ya Nachingwea, Lindi.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 25, 2021 baada ya kukagua mradi huo kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Lindi.

“Watu wote waliohusika na wizi wa nondo za ujenzi wa mradi huu wachukuliwe hatua haraka kwani tusipoanza kuwabana watu leo, wakatambua wajibu wao wa kuwatumikia wananchi miradi mingi ya maendeleo haitakamilika.”

Aidha Waziri Mkuu amemuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Dkt. Charles Mtabo kuwa makini katika usimamizi na uendeshaji wa shughuli za sekta ya afya wilayani humo ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu sekta hiyo yanafikiwa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea Dkt. Ramadhani Maiga amesema mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili unatekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na mfuko wa jimbo kwa gharama ya shilingi milioni 184.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezungumza na madiwani, watumishi wa umma na wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Nachingwea na kuwasisitiza kila mmoja atambue kwamba yupo wilayani Nachingwea kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo atimize majukumu yake ipasavyo.

Waziri Mkuu amesema jukumu lake ni kuona kila agizo la Rais Mheshimiwa Samia linatekelezwa, ambapo amewataka watumishi hao wa umma wahakikishe uwajibikaji wao unakuwa na matokeo chanya.

Hata hivyo ametoa rai kwa Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea wasimamie vyanzo vyote vya mapato na wahakikishe fedha zote zinazokusanywa zinaingia kwenye mfuko wa halmashauri.

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Maafisa Mifugo nchini watenge muda wa kwenda kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu namna bora ya ufugaji ili kuondoa migogoro na uvamizi wa mifugo kwenye mashamba ya wakulima kwani hakuna sababu ya wananchi kulalamika kwenye sekta ambayo wanasimamia.

Waziri Gwajima asisitiza mifumo rafiki ya kiutendaji
IS wahusika na ugaidi Uganda