Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wataalam wa malikale kutumia teknolojia ili kuhakikisha zinatumika katika kuinua uchumi wa nchi.

Akizungumza jana wakati akifungua mkutano wa Kimataifa wa siku nne unaojadili Uhifadhi wa Urithi wa Dunia wa Afrika kama Nyenzo ya kuleta Maendeleo Endelevu ulioanza jijini Arusha, Waziri Mkuu alisema kuwa endapo teknolojia itatumika kusaidia uvunaji wa gesi asilia na madini bila kuathiri uhifadhi wake, itasaidia kuondoa umasikini.

“Tunatambua umuhimu wa kutunza rasilimali na vivutio vya urithi asilia. Hivi ni kwa nini zisitafutwe teknolojia zinazofaa ambazo zitaruhusu uvunaji wa gesi asilia na madini bila kuathiri uhifadhi wa vivutio vya urithi asilia wa dunia (world heritage sites)?”, alihoji Waziri Mkuu.

“Serikali za nchi za Kiafrika zinahitaji suluhisho kama hili wakati zikiendelea kutafuta njia sahihi za kuwianisha uhifadhi wa vivutio vya urithi wa dunia na changamoto ya kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” aliongeza.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi na maliasili kama madini, misitu, wanyama na maeneo ya kihistoria ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuvilinda na kuvitunza.

“Tukizitunza rasilimali zetu zitasaidia kupata mapato kutokana na utalii Serikali itapeleka sehemu ya mapato haya katika miradi mbalimbali na hivyo kuchangia kwenye pato la Taifa,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na UNESCO hasa katika masuala yanayohusu uhifadhi wa vivutio vya dunia kutokana na umuhimu wake kwenye maendeleo endelevu.

Mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 150 kutoka nchi mbalimbali duniani, unajumuisha washiriki kutoka nchi 36 zikiwemo nchi 12 ambazo ni za nje ya bara la Afrika.

Jerry Muro: Tunawafahamu Wanaoleta Figusu Figisu Za Uchaguzi
Mbeya City Kufanya Ziara Nchini Malawi