Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson leo, Aprili 12, 2020 ameruhusiwa kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa baada ya kubainika kuwa na virusi vya corona.

Waziri Mkuu huyo mwenye umri wa miaka 55, alilazwa kwenye Hospitali ya St Thomas ambayo iko jijini London ambapo alipatiwa matibabu kwa siku 10, siku tatu akiwa kwenye chumba cha watu mahututi (ICU).

Akizungumza kwenye kipande cha video kilichowekwa kwenye mtandao wa Twitter, Waziri Mkuu Johnson aliwashukuru wauguzi na madaktari kwa jinsi walivyomhudumia hata wakihatarisha maisha yao, akieleza kuwa “lolote lingeweza kutokea.”

Kwa mujibu wa Downing Street, kiongozi huyo atapumzika nyumbani hadi afya yake itakapoimarika.

“Kutokana na ushauri wa timu yake ya wataalam wa afya, Waziri Mkuu hatarejea kazini hivi punde. Anamshukuru kila mmoja katika hospitali ya St. Thomas kwa jinsi walivyomjali na kumhudumia. Mawazo yake yote ni kwa wale walioathirika na ugonjwa huu,” imeeleza.

Hali bado ni tete nchini Uingereza. Hadi kufikia leo, Aprili 12, 2020 watu zaidi ya 10,000 wamepoteza maisha kutokana na virusi vya corona.

Video Mpya: Waite – Esaya Feat Jazz Bee #support
CORONA: Marekani yaongoza idadi ya vifo na maambukizi