Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango ametoa shukurani kwa shirika la fedha duniani, (IMF) kwa kusamehe deni ambalo walikuwa wanaidai Tanzania la takriban Bilioni 33.

Ametoa shukurani hiyo leo Juni 11, Bungeni jijini Dodoma alipokuwa anawasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21 na kusisitiza kuwa wanaendelea kuomba mashirika mengine yatoe msamaha wa madeni.

Hayo yamejiri baada ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) jana, kutangaza limeisamehe Tanzania deni lenye thamani ya Dola Milioni 14.3 (takriban Tsh. Bilioni 33) ambalo lilipaswa kulipwa ndani ya miezi minne ijayo, kuanzia Juni 10, 2020 hadi Oktoba 13, 2020.

IMF imechukua hatua hiyo kupitia mfuko wake wa ‘Catastrophe Containment and Relief Trust (CCRT)’ ili kuiwezesha Tanzania kukabiliana na athari za virusi vya Corona katika nyanja za kijamii na kiuchumi.

Taasisi hiyo imesema kutegemeana na uwepo wa fedha katika mfuko huo, huenda ikaongeza msamaha wa deni lenye thamani ya Dola Milioni 11.4 (takriban Tsh. Bilioni 26.4) ambalo linatakiwa kulipwa kati ya Oktoba 14, 2020 na Aprili 13, 2022.

IMF imeeleza kuwa janga hili limesababisha athari mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kupungua kwa watalii, changamoto za kibajeti na kupungua kwa makadirio ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) kutoka 6% hadi 4% katika mwaka huu wa fedha, na 2.8% katika mwaka wa fedha ujao

Ikumbukwe kuwa hatua hii imekuja ikiwa ni takribani miezi miwili tangu Rais wa Tanzania, Dkt Magufuli alipozitaka nchi zote za Afrika kuungana kuziomba taasisi za kifedha za kimataifa kutoa msamaha wa madeni badala ya kutaka kukopesha mikopo mingine.

Anayetajwa kutua Young Africans awaaga Rayon Sports
John Bocco: Tunajua ligi itakuwa ngumu, timu zote zimejiandaa