Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Mhe.Nape Moses Nnauye ameahidi kutoa shilingi  laki tano kwa kila goli litakalofungwa na timu ya Serengeti Boys  katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 utakaofanyika kesho katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Congo-Brazzaville.

Ameyasema hayo alipokua akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mhe.Nape amewakaribisha wadau wote wa michezo na wengine wanaopenda maendeleo ya mpira hapa nchini na kusema kuwa  milango ipo wazi  kujitolea katika kuiwezesha timu  kusonga mbele katika  mechi hii ambayo ni muhimu sana kushinda ili kufuzu kwa fainali hizo.

“Hii timu ni yetu sote hivyo inahitajika tuimiliki, tuipe nguvu, tuiombee ili iweze kufanya vizuri na hatimaye kufuzu kuingia fainali kwa kuitoa timu ya Congo-Brazzaville” alisema Mhe. Nape.

Hata hivyo aliongeza kuwa kesho asubuhi atakutana na wachezaji wa timu hiyo ili kuwapa maneno ya faraja kabla ya kuanza kwa mechi na amewataka  watanzania  kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa motisha wachezaji kwa kuwashangilia  na kuwatia moyo.

Mbali na hayo Waziri Nape alitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya kadi za kieletroniki zilizozinduliwa hivi karibuni kwa kueleza kuwa kadi hizo bado hazijaanza kutumika rasmi, zitaanza kutumiwa katika mchezo baina ya Wabunge wa Simba na Yanga pamoja na Bongo Fleva.

Timu ya Serengeti Boys inaundwa na vijana wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambapo katika mchezo wa kesho watahitaji ushindi na baadaye kucheza mechi ya marudiano mnamo Oktoba 2 mwaka huu nchini Congo-Brazzaville.

Makonda afungua ukurasa mpya Boda boda
Rais Mstaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi Aongoza Matembezi ya Hisani Kuchangia Wahanga wa Tetemeko la ardhi

Comments

comments