Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa mujibu wa sheria zilizopo na kutokuchukulia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kama mwanya wa kutokuwajibika kulipa kodi.

Mwigulu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Aprili 3, 2021 ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu kuteuliwa kwake kuongoza Wizara hiyo ambapo ameeleza yale ambayo Wizara imepanga kuyafanya ili kutekeleza maagizo ya Rais Samia kwa Wizara hiyo.

Mwigulu amesema ili nchi iweze kuendelea na kupata mapato makubwa ni lazima ikuze uchumi, hivyo Wizara hiyo imepanga kutengeneza walipa kodi wapya kwa kutumia wataalamu na kuhakikisha hawaui walipa kodi waliopo kama ambavyo Rais Samia amesisitiza.

Aidha, Waziri Nchemba ameonya tabia ya Mamlaka ya Mapato (TRA), kukadiria wafanyabiashara kodi kwa kipindi kirefu na kuitaka mamlaka hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia shria na weledi katika sekta ya ukusanyaji wa mapato.

“Inatokea mtu ameshakadiriwa miaka yote kodi, na amepewa clearance, amepewa cheti kwamba huyu tumemkadiria na amelipa, inapita miaka kumi anaenda kukadiriwa tena, analipa, akiwa anajua haya yameisha anaelekea kwenye shughuli na uzalishaji anaambiwa alete taarifa ya miaka 10 au miaka 15, hii tuache, tufuate taratibu za sheria zetu tulizotunga za namna ya kufanya ukadiriaji,” amesisitiza Waziri Nchemba.

“Utaratibu ambao upo unahusisha ofisi pamoja na mhusika anapewa certificate (cheti) cha mwaka hadi mwaka, anakuwa cleared mwaka hadi mwaka,” amefafanua Waziri Nchemba.

Waziri Nchemba ameielekeza TRA kuzingatia maelekezo ya Rais Samia na kuacha kushika akaunti na fedha za wafanyabiashara.

Wakenya wapigwa marufuku kwenda Uingereza
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 3, 2021