Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Mwigulu Nchemba, amewataka wakuu wa mashirika ya umma na taasisi binafsi nchini kuacha tabia ya kuwaingilia  Wakaguzi wa ndani katika utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri Nchemba, ameyasema hayo  jijini Arusha, wakati akifungua mkutano wa nane wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), huku akielezea umuhimu wa wakaguzi wa ndani wamekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya nchi lakini wanasaidia kuangalia kasoro zote zinazojitokeza kabla ya wakaguzi wa nje.

“Wakaguzi wa ndani hasa wa serikali wamekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo kwa kuwa wapo ndani ya ofisi za umma na wanaweza kuzuia upotevu wa fedha katika mashirika na taasisi zao,”Amesema Waziri Nchemba.

Aidha Nchemba amesema awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa anapokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),alitoa mwelekeo wa serikali yake, kuwa wakaguzi wote wa hesabu za serikali hawapaswi kuficha kitu chochote bali wanatakiwa kukagua kwa ujasiri kwa ajili ya kulinda fedha za wananchi.

Hata hivyo Wizara ya Fedha na Mipango imeahidi kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na taasisi hiyo ili iweze kutimiza majukumu yao ipasavyo lakini pia watumishi kupata mafunzo.

Naye Mkurugenzi Mkaguzi wa Benki ya Maendeleo Tanzania(TIB),Christine Mbonya, amesema kuwa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Fedha kwa Wakaguzi wa ndani watakwenda kuyafanyia kazi kwa kuwa amewapa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii, kwa maarifa zaidi na kwa kutokuogopa.

Kwa upande wake Rais na Mwenyekiti wa IIA, Anna Victor, amesema kuwa, wamepokea vizuri kauli ya Waziri Dk.Nchemba kwamba wakafanye kazi bila ya kuwa na hofu na pale panapotokea kasoro waseme ukweli na kuweka wazi.

PSG kumkosa Messi
FC Barcelona kumpa muda Koeman