Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya kutajwa katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi iliyoonyesha namna serikali lilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.

Waziri Simbachawene ameandika barua hiyo muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwataka viongozi wote aliowateua na wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni ili kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.

Mbali na Simbachawene, wengine waliokuwa wametakiwa kukaa pembeni ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani

Rais Magufuli amewataka wateule wake wote waliotajwa katika ripoti za kamati zilizotathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya tanzanite na almasi kukaa pembeni kupisha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zake.

Rais Magufuli amesema hayo leo Septemba 7, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea ripoti za kamati hizo zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Ripoti za kamati hizo zimewataja baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, James Mdoe; Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani.

Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema alikuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua mawaziri waliotajwa jana Septemba 6 alipokabidhiwa ripoti ya kamati hizo lakini hakufanya hivyo na badala yake aliamua ripoti ziwasilishwe kwa Rais John Magufuli ambaye ni mwanzilishi wa suala hilo ili liwe wazi zaidi.

Waziri Mkuu, Majaliwa amesema alipendekeza ripoti hizo zikabidhiwe kwa Rais Magufuli ili kuendeleza utaratibu wa kuyaweka mambo hayo wazi na kuwaeleza ukweli Watanzania.

Wenger: Hakuna kilichoharibika, mambo ni shwari
JPM awakaanga waliotajwa kwenye ripoti ya madini