Serikali kupitia Wizara ya Afya, imesema kwa sasa hali ni salama mkoni Kagera kufuatia ziara ya katika kijiji cha Ntoma Wilaya ya Bukoba Mkoani humo kwa lengo la kujionea hali inavyoendelea baada ya kutangazwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu mara baada ya kufika katika kijiji cha Ntoma akiambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi wa Shirika la UNICEF, Shalini Bahuguna.

“Niwatoe hofu Watanzania tuendelee kufanya kazi zetu lakini tuzingatie maelekezo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kuepuka kushikana mikono hususan kipindi hiki lakini pia tujitahidi kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni,” amesema Waziri Ummy

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Zabron Yoti (wa kwanza kulia), Mwakilishi wa Shirika la UNICEF Shalini Bahuguna (wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima (wa kwanza kushoto)

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo unamalizika na hautatokea tena katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kanyangele Hamim Hassan ameishukuru Serikali kwa kufanya juhudi kubwa ambapo hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeongezeka kwa kuthibitika kuwa na ugonjwa huo.

“Hatua za Serikali kupitia Wizara ya Afya zilizochukuliwa za kuwaweka sehemu maalumu waliokuwa karibu na wagonjwa imesaidia sana kutoendeleza maambukizi kwingine na hali ni shwari kwa sasa.” amesema Hassan.

Maandamano Kenya: Polisi yatema cheche
Mwaibula: Mteule wa Mkapa, mwanzilishi ruti za Daladala