Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Deni la Taifa ni himilivu.

Dkt Mwigulu amesema hayo leo Jumanne Januari 4, 2021 Ikulu wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.

Amesema kutokana na tathimini iliyofanyika mwezi Novemba mwaka 2021 inaonyesha kuwa deni hilo ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Tathimini ya uhimilivu wa deni uliofanyika Novemba kama ulivyoelekeza Mhe. Rais, unaonyesha deni letu ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu,” amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mwigulu amesema kwa sasa bado nchi ipo kwenye nafasi nzuri kufikia kwenye kikomo cha deni kidunia.

“Katika tathimini hiyo viashiria vinaonyesha kwamba, deni la Serikali kwa uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 31 ambapo ukomo wa kidunia ni asilimia 55,” aliongeza.

Katika hatua ya kuelezea ukamilishaji na utekelezaji wa fedha za IMF Waziri Mwigulu amesema kuna kiasi cha fedha hizo zimeondolewa riba kutokana na utekelezaji wake kufanyika kwa ufasaha.

“Mh Rais hatua hiyo ya utekelezaji wa fedha hizo iliendelea na imeongeza imani kubwa kwa viongozi wa IMF, na kuamua kufuta masharti yote yaliyokuwa na riba kwa upande wa fedha za dirisha la ‘rapid financing instrument’ ambayo ilikua sawa na theluthi mbili ya mkopo wote. Hivyo napenda kuwafahamisha watanzania kuwa mkopo wote wa dola milioni 567.25 sawa na trilioni 1.3 utakua mkopo usio na riba na hautalipiwa riba, hivyo fedha tulizochukua tutarudisha hivyo hivyo,” alisema Dkt Mwigulu.

Oktoba 10, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19.

Hii leo tarehe 04 Januari, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19, Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Nchemba ashusha 'nondo' za deni la Taifa, mkopo
Dkt. Mwigulu ataja zilipoenda fedha za tozo za miamala