Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umeitaka klabu ya soka ya Etoile Du Sahel ya nchini Tunisia kuhakikisha inawalipa mapema fedha za aliyekuwa mchezaji wao Emmanuel Okwi  kabla ya kufikia mwezi Machi mwakani.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa klabu hiyo Haji Manara amesema klabu hiyo ya Etoile Du Sahel iliandika barua kwenda Shirikisho la soka la Dunia FIFA kutaka kuongezewa muda wa kulipa deni lao ndani ya klabu ya Simba hadi mwezi Machi mwakani, jambo ambalo uongozi wa Simba umepinga suala hilo.

Klabu ya Simba inaidai klabu ya Etoile Du Sahel takribani sh. milioni 600 kwa ajili ya mchezaji wao Emmanuel Okwi ambazo hazijalipwa hadi sasa ndani ya klabu hiyo.

“Imekuwa ni tabia yao kutuzungusha, kila unapokaribia muda wa kulipa deni huandika barua FIFA na kuomba waongezewe muda.Tumeshachoshwa na hali hii”

Okwi alinunuliwa na Etoile Januari mwaka 2013 kwa dau la dola 300,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 600 za kitanzania ingawa baada ya muda akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo ya Tunisia.

Mtafaruku ulianza baada ya Okwi kuchelewa kurejea mjini Sousse mkoani Sahel baada ya ruhusa ya kwenda kuichezea timu yake ya taifa, Uganda.

Okwi naye akadai Etoile walikuwa hawamlipi mishahara na kufungua kesi FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), ambayo mwisho wa siku alishinda kwa kuruhusiwa kutafuta timu nyingine ya kuchezea kulinda kipaji chake, wakati akisubiri suluhisho la mgogoro wake na klabu ya Tunisia.

Hata hivyo, Okwi  mwaka huu Simba ilimuuza katika klabu ya Sonderjyske FC inayoshiriki  Ligi Kuu ya Denmark ambako amesaini mkataba wa miaka mitano.

Leicester City Wabanana Na Manchester City
Ndege yagonga jengo na kuanguka katikati ya Mji wa Marekani