Msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu amezua kizaa zaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akigoma kukamatwa na polisi baada ya mahakama hiyo kumwachia huru na kisha kumkamata tena na kumuweka mahabusu ya mahakama hiyo.

Wakati askari wakimkamata kwa nguvu, Wema aligoma kukamatwa hali iliyosababisha mvutano kwa muda kati askari na mawakili wake, Albert Msando na Reuben Simwanza.

Aidha, askari hao walifanikiwa kumkamata msanii huyo aliyekuwa Mahabusu ya Gereza la Segerea ambapo alifika mahakamani asubuhi kwa ajili ya kusikiliza kesi yake inayoendelea mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Glory Mwenda amedai hana shahidi baada ya shahidi aliyemuandaa, Koplo Safi kudai ni mgonjwa.

Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa Wema, Albert Msando kwa madai kwamba haina mashiko, mahakama ilishatoa ahirisho la mwisho hivyo hawawezi kuahirisha tena.

“Mheshimiwa shauri lipo zaidi ya siku 60, upande wa mashtaka wameshindwa kuleta mashahidi, tunaomba chini ya kifungu namba 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 mshtakiwa aachiwe huru,” amedai Msando.

Wakili Mwenda alipinga akidai sheria ya siku 60 inatumika pale tu ambapo upelelezi haujakamilika hivyo aliomba kesi iahirishwe.

Hakimu Kasonde alisema anakubaliana na maombi ya upande wa utetezi, sheria hiyo inatumika wakati wowote hivyo mahakama inamuachia huru mshtakiwa.

Wema anakabiliwa na mashtaka ya kusambaza video ya ngono katika mitandao ya kijamii kupitia simu yake ya kiganjani.

Ashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumlawiti mama yake mzazi
Wachimbaji wawili wafariki dunia kwa kufukiwa na kifusi

Comments

comments