Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger, amekanusha taarifa za kuwa kwenye mpango wa kumuweka sokoni mshambuliaji wake kutoka nchini Chile, Alexis Sanchez, ambaye bado hajathibitisha kama atasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia The Gunners.

Wenger amekanusha taarifa hizo, kufuatia uvumi unaoendelea kusambaa kuhusu mustakabali wa Sanchez ndani ya kikosi cha Arsenal, ambapo zinaeleza kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwa mshambuliaji huyo akaondoka katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Wenger amesema anaamini mshambulaiji huyo mwenye umri wa miaka 28 ataendelea kuwa sehemu ya kikosi chake msimu huu na misimu ijayo, licha ya kuendelea kumbembeleza akubali kusaini mkataba mpya.

“Hakuna ukweli wa jambo hilo linalozungumzwa, tuna maelewano mazuri na Sanchez, na nina uhakika ataendelea kubaki Emirates Stadium kwa msimu huu na misimu mingine ijayo,” Wenger aliiambia Sky Sports News HQ.

Alipoulizwa kama kweli Sanchez aliwahi kumwambia anahitaji kuondoka klabuni hapo, babu huyo wa kifaransa alisema, “Haijawahi kutokea.”

“Hakuna anaejua kama Sanchez ataitumikia Arsenal kwa msimu wa mwisho, kwa sababu kuna uwezekano wa mazungumzo yetu yakazaa matunda na mwishowe akasaini mkataba mpya kabla au kati kati ya msimu,” alisema.

Klabu ya Manchester City imeendelea kutajwa katika harakati za kumuwania mshambuliaji huyo aliyekua miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi cha Chile wakati wa fainali za kombe la Mabara nchini Urusi, na dhumuni kubwa linalolengwa hapo, ni mchezaji huyo kujiunga na aliyewahi kuwa meneja wake akiwa FC Barcelona Pep Guardiola.

 

Wananchi 121 wa Uganda watoweka
Donnarumma amwaga wino mpya AC Milan