Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amewasihi mashabiki wa klabu hiyo kutoingia na hofu ya kushindwa kumaliza katika kilele cha kundi la kwanza la michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Wenger amesema matokeo ya sare ya mabao mawili kwa mawili dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG, huenda ikawa imebadilisha matarajio ya mashabiki wengi wa klabu hiyo duniani kote, lakini kwake anaamini mapambano bado yanaendelea.

Babu huyo amesisitiza kuwa, soka ni mchezo wa kushindana hadharani na timu yao imekua ikionyesha mchezo mzuri tangu mwanzoni mwa msimu huu, hivyo hakuna litakaloshindikana katika michezo miwili iliyosalia ya hatua ya makundi wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Ludogorets Razgrad na FC Basel.

Sare ya usiku wa kuamkia hii leo, inachukuliwa kama faida kwa PSG ambao wanapewa nafasi kubwa ya kumaliza wakiwa kileleni mwa kundi la kwanza, kutokana na udhaifu wa timu pinzani.

Kwa sasa msimamo wa kundi la kwanza unaonyesha Arsenal na PSG wana point 11 kila mmoja huku wakizidiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Arsenal wana tofauti ya mabao 9 ya kufunga na kufungwana PSG wana tofauti ya mabao 6 ya kufunga na kufungwa.

Katika mchezo wa usiku wa kuamkia hii leo, mabao ya Arsenal yalifungwa na Olivier Giroud na Marco Verratti baada ya kujifunga huku mshambuliji Edinson Cavani akiifungia bao la kwanza la PSG kabla ya Alex Iwobi kujifunga mwenyewe.

Ifahamu Siri Ya Kadi Za Njano Mwishoni Mwa Mwaka
Ligi Ya Mabingwa Barani Ulaya