Serikali imetoa agizo kwa mameneja wote wa mikoa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha viwanda vyote nchini vinafungiwa Transfoma mahsusi kwa matumizi ya viwanda pekee pasipo kuchanganya na matumizi ya wananchi.

Agizo hilo limetolewa mkoani Kagera na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati akizungumza na Uongozi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo (SIDO), mkoani humo, mara baada ya kukagua Transfoma mpya iliyofungwa maalumu kwa matumizi ya Shirika hilo.

Dkt. Kalemani amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda hivyo na kuviwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Wenye viwanda wawe na Transfoma zao, wasichangie matumizi na wananchi. Mwananchi akiunguza kwake anaathiri Kiwanda pia maana umeme utakosekana kote hivyo uzalishaji unasimama. haifai.”amesema Dkt. Kalemani

Pia amewaagiza mameneja nchi nzima kuhakikisha wanabadilisha miundombinu yote ya umeme ambayo ni mibovu katika maeneo yao mathalani Transfoma, Nguzo, Nyaya na Mita ili kuwaondolea wananchi kero za kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Aidha, amesema kuwa miundombinu iliyoharibika isiporekebishwa kwa wakati, husababisha shirika kupoteza mapato hivyo kuitia hasara Serikali.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani ametembelea na kukagua uunganishwaji umeme katika Taasisi ya SIDO eneo la Rwamishenye na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) Tawi la Bulugo wilayani Bukoba, ambapo amekiri kufurahishwa na utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kwa uongozi wa TANESCO, kuzifungia Taasisi hizo Transfoma.

 

Waziri Makamba awatoa hofu Watanzania
Fahamu namna mwili unavyofaidika na maji ya madafu