Wenyeviti wa Serikali za mitaa Kata ya Kivavi mjini Makambako wamegoma kushiriki kikao cha kujadili maendeleo ya Kata hiyo (Kamaka) kwa kile kilicho elezwa kuwa ni kutokana na diwani wao kutokuhudhuria vikao.

Wakizungumza na Dar24 wenyeviti hao wamesema kuwa diwani wa kata hiyo, Baraka Kavambe ameshindwa kuhudhuria takribani vikao vinne pasipo kuwa na sababu za msingi, hali ambayo imepelekea shughuli za kimaendelo kukwama ndani ya Kata hiyo hususani ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Deo Sanga.

“Tumefika hivi leo ni kwasababu ya madarasa watoto wetu wapo nje hawana pa kuingia lakini cha ajabu tangia tunaanza hii shughuli hatumuoni diwani tunamuona kaimu diwani tu hatujui sababu nini mpaka hashiriki kikao kwa hiyo sisi hatuwezi kushiriki kikao cha leo mpaka tumuone diwani na sasa ni vikao vinne hajashiriki vikao” wamesema wenyeviti.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Sigridi, Mathias Mdage ambaye ndiye amekuwa akizungumza kwa niaba ya diwani huyo amewataka wenyeviti wenzake waendelea kufanya kazi ili kukamilisha shughuli hiyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kua diwani anamatatizo ya kifamilia na baada ya siku 60 atarudi kazini.

“Wakati nakaimishwa diwani aliniaga kuwa na matatizo ya kifamilia kwa hiyo nimshikie nafasi yake, niwashukuru wenyeviti tangu tumeanza kikao cha kwanza tulianza kufanya vizuri na hili jambo la ujenzi wa shule limekuja kunikuta wakati mimi nimekaimu na tumeendelea kushirikiana na wenyeviti vizuri niwaombe tu wenzangu tuendelee kushirikiana kuchapa kazi” alisema Mdage

Akifafanua kuhusiana na kitendo cha kukaimisha nafasi ya udiwani, Mwenyekiti wa halmashauri mji Makambako ambaye pia ni diwani wa kata ya Maguvani, Hanana Mfikwa amesema kuwa kutokana na kanuni ambazo zipo, diwani harusiwi kukaimisha mtu mwingine nafasi yake.

“Ilitakiwa kama diwani hayupo wanamchagua wao wajumbe, mwenyekiti wa kikao hicho hachaguliwi na diwani kukaimishwa maana kikao hicho hakikaimishiki, angekuwepo diwani wa viti maalumu ndio angeendesha hicho kikao kwa niaba ya diwani, hapo ilitakiwa wamchugue mwenyekiti wa kikao kwa niaba ya wenyeviti waliopo tena hapo walifanya makosa sana na hicho kikao kweli hakikuwa halali” alisema Mfikwa

Video: Gambo apongeza mradi wa TACIP, asema unafuta kilio cha wasanii
HapoKale: 'Wenye kulamba' hadi kuwa Wanyiramba