Wagonga nyundo wa London West Ham United, wameanza mazungumzo na wakala wa mshambuliaji kutoka nchini Italia Simone Zaza, ili kuangalia uwezekano wa kumsajili moja kwa moja kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 20.

Gazeti la The Sun limeripoti kuwa, The Hammers hawapo tayari kulipa kiasi hicho cha pesa ambacho kinapaswa kupelekwa kwa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus, ambao walikubali kumtoa Zaza kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu.

Sehemu ya mkataba wa mkopo wa Zaza mwenye umri wa miaka 25, unaelekeza malipo hayo ya Pauni milioni 20, endapo atatumika katika michezo 14 akiwa na West Ham Utd na mpaka sasa ameshacheza michezo 10 (8 ikiwa ya ligi).

Hata hivyo chanzo cha habari kutoka ndani ya klabu ya West Ham Utd kimeliambia gazeti la The sun kuwa, hawapo tayari kulipa kiasi hicho cha pesa kutokana na uwezo wa mchezaji huyo kutowaridhisha.

“Kwa sasa tupo katika harakati za kufanya mazungumzo, lakini kiukweli hatujaona cha ajabu kutoka kwa mchezaji huyo ambaye tuliamini huenda angetusaidia katika msimu huu wa ligi.” Kimeeleza chanzo hicho

“Tunahitaji kuwashusha hadi kufikia katika kiwango cha pesa ambacho tunaamini kitalingana na uwezo wa Zaza, lakini sio kwa Pauni milioni 20.” Kiliongeza chanzo hicho.

Zaza huenda akacheza katika mchezo wa robo fainali wa kombe la ligi dhidi ya Manchester United hapo kesho.

“Michezo ya kombe la ligi haihesabiwi kutokana na makubaliano yetu, inayotambulika kimkataba ni michezo ya ligi pekee” Chanzo cha habari kilitoa ufafanuzi huo.

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, Zaza amekua katika mawindo makali ya klabu za nchini kwao Italia Napoli na AC Milan, na kama mambo ya kusajiliwa moja kwa moja yatashindikana huenda akaondoka mwezi Januari wakati wa dirisha dogo la usajili.

Gareth Southgate Kusaini Mkataba Wa Miaka Mitatu
Possi aitaka jamii kuwa kwamua wenye ulemavu