Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula kaskazini mwa Ethiopia imeongezeka na kufikia takriban watu milioni 9.4 na hii ni kutokana na vita inayoendelea nchini  humo,

Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi shirika hilo limesema eneo la Amhara ambapo mapigano makali yanaendelea idadi ya watu wenye uhitaji imepanda kwa kasi na kufikia watu milioni 3.7 ambao wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. 

Taarifa hiyo imesema “katika watu wa Kaskazini mwa Ethiopia wanaohitaji msaada zaidi ya asilimi 80 au sawa na watu milioni 7.8 wako katika eneo ambalo ni uwanja wa mapambano na hivyo ni muhimu sana msaada wa chakula uweze kuvuka uwanja wa mapambano na kuzifikia familia zenye uhitaji.” 

Kwa mujibu wa WFP wiki hii imefikisha msaada wa chakula kwa watu zaidi ya 10,000 kwenye miji ya jimbo la Amhara ya Dessie na Kombolcha kwa niaba ya operesheni ya dharura ya pamoja (JEOP). 

Huu ni usambazaji wa kwanza wa mgao wa chakula tangu miji hiyo iliponyakuliwa na vikosi vya Tigray yapata mwezi mmoja uliopita, kwani WFP ilipewa fursa ya kufikia ghala lake kwenye eneo hilo wiki iliyopita. 

Kuhusu hali ya lishe kote Ethiopia Kaskazini WFP inasema inazidi kuzorota huku takwimu za uchunguzi kutoka mikoa yote mitatu zikionesha viwango vya utapiamlo kati ya asilimia 16%-28% kwa watoto.  

La kutisha zaidi, ni kwamba hadi asilimia 50% ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha waliochunguzwa huko Amhara na Tigray pia walipatikana kuwa na utapiamlo. 

Hadi sasa WFP imefikia zaidi ya watu milioni 3.2 kwa msaada wa dharura wa chakula na lishe kote kaskazini mwa Ethiopia, ikiwa ni pamoja na akina mama na watoto 875,000 walio katika mazingira magumu na kuwapatia chakula kilichoimarishwa kwa lishe bora katika jimbo la Tigray na Amhara. 

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 27, 2021
Marufuku kutoa taarifa za harakati za kijeshi Ethiopia