Mwimbaji wa Bongo Fleva, Whozu ameweka wazi kuwa alinyolewa nywele na kutishiwa kupigwa risasi na aliyekuwa mpenzi wa mrembo Tunda aitwaye Ali, baada ya kuwakuta wakiwa chumbani kwa mrembo huyo jijini Dar es Salaam usiku wa manani.

Msanii huyo ameeleza kuwa alianza uhusiano na Tunda baada ya kumueleza kuwa ameachana na mpenzi wake. Aidha, alisema kabla ya kupata kauli hiyo ya Tunda, alikuwa ameshapigana na huyo jamaa mjini Moshi kutokana na ugomvi ulioibuka kwa sababu ya wivu wa mapenzi.

Ameeleza kuwa Februari 25 mwaka huu alikuwa nyumbani kwa mrembo huyo maeneo ya Mbezi, ambapo akiwa na rafiki zake ‘Wabantu’ ambao walienda kwa ajili ya kuangalia filamu, walikaa hadi usiku wa manani na wakaamua kulala.

Mkali huyo wa ‘Huendi Mbinguni’ ameeleza kuwa yeye alilala na Tunda chumbani lakini ghafla nyumba hiyo ilivamiwa na watu wapatao sita ambao waliruka ukuta, wakavunja mlango hadi wa chumbani na kuwapiga wote waliokuwa ndani. Watu hao kwa mujibu wa Whozu waliongozwa na hasimu wake katika penzi la Tunda, Ali.

Ameeleza kuwa wakati akijaribu kujitetea kwa kupigana na watu hao waliokuwa na silaha za jadi yakiwemo mapanga na marungu, hasimu wake huyo alitoa bastola na kumuelekezea kichwani akitishia kumpiga risasi, ndipo alipoamua kuwa mpole.

Amedai baada ya kutulia, mtu huyo alimtaka mmoja kati ya wenzake waliovamia kumkata nywele, na ndipo amri hiyo ilipotekelezwa wakati yeye akiwa mpole akihofia kupigwa risasi.

“Jamaa ndio akanichomolea bastola… ilibidi niwe mpole kwa sababu kile ni kifaa ambacho ni cha hatari, muda wowote anaweza kuniua au anaweza kunitoa kilema. Kwahiyo mimi kupigana naye tena ilibidi nitulie, nilipotulia akaendelea kuninyoshea bastola na kunitukana,” Whozu amefunguka kwenye mahojiano maalum na Dozen Selection.

“Nilikuwa mpole, hapo ndipo alipopata nafasi wakanishika nywele na kuninyoa kwa sababu nywele zilikuwa wazi nilikuwa nimeziachia tu sikuzifunga kitambaa. ‘Au ndio nywele zako zinakupa kiburi?’ aliniuliza.

“Sikuweza kumjibu… na wadogo zangu pia walikuwa wapole, basi wakaleta panga wakati huo Tunda naye akiwa pembeni analia kwa sababu walimpiga, wakakata nywele… ila hakukata yeye, alikata mshikaji wake ila yeye akawa amewashikia rasta,” aliongeza.

Msanii huyo ameeleza kuwa aliripoti tukio hilo polisi ambapo alipewa ushirikiano wa kutosha, hivyo anaamini sheria itachukua mkondo wake.

Waliotuhumiwa kuwa magaidi wa ISIS, Al-shabaab watupwa jela Rwanda
Wafungwa wamiliki simu Gerezani

Comments

comments