Leo ni siku ya Maji Duniani, ambapo hitaji hilo ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama, huku Baadhi ya Wananchi wakisema kila mwanadamu anapaswa kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu.

Wakizungumza na Dar24 Media, baadhi ya Wananchi na Wadau wamesema haki ya Maji safi na salama, ni kati ya changamoto kubwa katika ulimwengu kwani kuna baadhi ya nchi ambazo zinapinga maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu lakini ukweli ni kwamba Maji ni uhai na kikolezo cha maendeleo.

Mmoja wa Wananchi hao, Tadi Mpilimi anasema, “kila kukicha hitaji la Maji safi na salama linaendelea kuongezeka maradufu sehemu mbalimbali Duniani, ni sehemu ya haki za msingi za Binadamu na kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama na yenye ubora.”

Naye Rehema Daniel, mmoja wa akina mama ambaye ni mjasiriamali msomi wa chuo kikuu anasema “rasilimali maji, inapaswa kushughulikiwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika sera za kitaifa na kimataifa kutokana na umuhimu wake kwa maisha ya binadamu kwani hii ni sehemu muhimu katika mchakato wa maboresho ya maisha sanjari na mapambano dhidi ya umasikini.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Youth Era Foundation, John Kanola amesema “sera hizi anazozisema Dada Rehema ziwe na mwelekeo wa kisiasa na kisheria, kama ilivyokubaliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2010, wadau wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, kwani hii ni sehemu ya mustakabali wa binadamu kwa siku za usoni.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani, hivyo Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote.

Serikali kutenga fedha ulindaji hadhi ya urithi Zanzibar
Fiston Mayele: Sitarudi tena Tanzania