Serikali inaendelea kutangaza Kimondo kilichopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya ikiwa ni kivutio muhimu na adimu nchini na duniani kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Kamani leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa  Mhe. Japhet Hasungu lililohusu mpango wa Serikali katika kuhamasisha watalii wa ndani na nje kuja kuangalia Kimondo hicho.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali imekuwa inaendelea kuhamasisha kwa kukitangaza Kimondo hicho kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo vipindi vya runinga na nakala za machapisho mbalimbali.

“Uhamasishaji umefanyika kwa kutumia njia mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na vipindi vya runinga vya ZAMADAMU na Utalii wa ndani na kutumia machapisho ya Tanzania ya “The land of great Heritage Sites” na “Tanzania Cultural Heritage Resources” ambapo nakala zake husambazwa katika maonesho mbalimbali na Balozi zetu pamoja na jarida la “Ifahamu Idara ya mambo ya kale”” na jarida la Maliasili,” alifafanua Naibu Waziri huyo.

Aidha, Mhandisi Kamani aliongeza kuwa juhudi hizo limepelekea ongezeko la idadi ya watalii na mapato ambapo kati ya mwaka 2012/2013 na 2014/2015 watalii waliongezeka kutoka 990 hadi 1,681 pamoja na mapato kuongezeka kutoka shilingi 811,000 hadi 2,426,00.

Mbali na hayo, Mhandisi Kamani alitoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na wadau wengine kujitokeza kuboresha mazingira na miundombinu ya eneo la kimondo hicho ili kuweza kuzidi kuvutia watalii wengi na kuongeza pato la taifa.

Kimondo hicho kinaendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia katika masuala ya utalii ambapo kinaaminiwa kuwa ni kati ya vimondo nane vikubwa zaidi duniani kinachokadiriwa kuwa na uzito wa tani 12, urefu wa mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22.

Mgodi wa Dhahabu Geita Gold Mine Watoa Milioni 444 Kwaajiri Ya Kuchangia Madawati Mkoani Geita
Serikali Yaunda Timu ya Wataalamu wa Kutatua Migogoro ya Ardhi Nchini