Bingwa wa masumbwi wa dunia uzito wa juu, Deontay Wilder  amekataa kuhudhuria pambano kati ya hasimu wake Anthony Joshua na Joseph Parker licha ya kuahidiwa pesa nyingi na Sky Sports.

Wilder amedai kuwa ingawa alipewa dili la kuwa kati ya timu ya watangazaji wa Sky Sports katika pambano hilo litakalofanyika Jumamosi hii usiku nchini Uingereza, amechukizwa na hatua ya kukatazwa kupanda ulingoni na kumpa ujumbe wake Joshua uso kwa macho.

Mbabe huyo alidai kuwa alipopewa nafasi hiyo aliuliza kama ataruhusiwa kupanda ulingoni kama Joshua atashinda, ampe ujumbe wa ‘kibabe’ kuwa atampiga kwa KO katika pambano lao na alikubaliwa.

Hata hivyo, alidai kuwa hivi karibuni, alipigiwa simu na promota wa pambano hilo ambaye alimwambia kuwa Joshua amekataa mpango huo na kwamba ametaka kuongeza ulinzi zaidi.

“Nimeambiwa Joshua amekuwa akizungumza kuwa hataki kuniona ulingoni, anazungumzia kuongeza ulinzi. Nimesikia hata kitu kama kutafuta amri ya mahakama ya kunizuia kumsogelea,”alisema Wilder.

Mpiganaji huyo alidai kuwa kitendo cha yeye kupanda ulingoni na kumuangalia Joshua usoni kingeongeza hamasa ya pambano lao lijalo.

Akijibu madai ya Wilder, promota wa pambano hilo, Eddie Hearn amekiri kuwa walizungumzia mpango huo lakini walimtaka asichukulie kuwa ni lazima.

Hearn alisema kuwa walimueleza Wilder kuwa itabidi asubiri hadi Joshua atakapomuita apande ulingoni, ndipo afanye hivyo, vinginevyo haitawezekana, sharti ambalo hakulikubali.

Watu 78,000 wanatarajiwa kushuhudia pambano hilo katika uwanja wa mpira wa Principality ambao ni wa nne kwa ukubwa nchini Uingereza.

Joshua atapanda ulingoni akiwa na rekodi ya kushinda kwa KO katika mapambano yake yote 20 na Parker atakuwa na rekodi ya kutopoteza pambano hata moja katika mapambano yake 24.

 

Liverpool, Man Utd kukutana Marekani
John Stones kuikosa Everton