Mshambuliaji Wilfried Zaha amesisitiza kutojutia maamuzi aliyoyachukua ya kuitema England na kukubali kurejea katika asili yake (Ivory Coast).

Zaha alifanya maamuzi ya kurejea kwenye asili yake mwishoni mwa mwaka jana, na atakuwa sehemu ya kikosi cha Ivory Coast kitakachoshiriki fainali za Afrika zitakazoanza mwishoni mwa juma hili nchini Gabon.

Mshambuliaji huyo alizaliwa mjini Abidjan mwaka 1992, alikua na ndoto za kucheza soka katika kikosi cha England na aliwahi kuitwa kwenye timu hiyo kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya kirafiki miaka mitatu iliyopita.

Zaha, alihamia mjini London akiwa na umri mdogo na alianza kujiendeleza kisoka katika nchi ya England.

Akizungumza na tovuti ya www.fedivoir.com alisema: “Nilikwenda England nikiwa na umri wa miaka minne, na sikuwahi kurejea nyumbani. Nilifanya kila jambo la kimaendeleo nikiwa huko.

“Sikukurupuka kufanya maamuzi ya kukubalia kurejea kuitumikia Ivory Coast, ilinichukua muda mrefu wa kufikiri na nilibaini kuna umuhimu wa kufanya hivi, kwa lengo la kurejesha mchango wangu kisoka kwa watu wa hapa.

“Ni jambo kubwa ambalo ninapaswa kujivunia, na katu sitajutia kufanya maamuzi ya kurudi kuitumikia Ivory Coast ambapo ndio asili yangu ilipo.”

Kocha wa sasa wa England Gareth Southgate, alijaribu kumshawishi Zaha kubaki katika himaya yake, lakini ilishindikana na hatimae alikubali kurejea Ivory Coast.

Kikosi cha Ivory Coast, leo kitacheza mchezo wa mwisho wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Uganda, kabla ya kusafiri kuelekea nchini Gabon tayari kwa michuano ya AFCON 2017, ambapo kitaanza kutetea ubingwa kwa kucheza na Togo Januari 16.

Eddie Howe Kumnusuru John Terry?
Maazimio Ya FIFA Yapingwa