Kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil na klabu ya Chelsea ya England Willian Borges da Silva, ameweka wazi matamanio yake ya kutaka kufanya kazi kwa mara nyingine tena na meneja Jose Mourinho.

Kiungo huyo amekua akihusishwa na mipango ya kutaka kusajiliwa na Man Utd katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi, huku uhusiano wake na Mourinho ukitajwa kuwa chachu ya mpango huo.

Willian amesema anafurahishwa kufanya kazi na meneja huyo kutoka nchini Ureno, na anaamini ipo siku katika maisha yake kabla hajaacha mchezo wa soka, jambo hilo litatimia.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa kauli ya kuhitaji kufanya kazi na Mourinho haihusiana na sakata linaloendelea hivi sasa la kuhusishwa na mpango wa kuihama Chelsea.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa ngao wa jamii dhidi ya Man City siku ya Jumapili, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, alisema: ” nimeshaweka wazi matarajio yangu, ninahitaji kucheza katika klabu ya Chelsea kwa hivi sasa, nina furaha hapa, sikuwahi kushinikiza suala la kutaka kuondoka.”

“Mourinho ni meneja ninaempenda, nilifurahia kufanya nae kazi alipokua Chelsea, ninatarajia kuna siku nitafanya nae kazi kwa mara nyingine tena, kabla sijaondoka katika tasnia ya mchezo huu,” Alisema Willian.

“Wakati mwingine tumekua tukitumia muda wetu kuzungumza kwa njia ya simu, tunachati na kila mmoja anamfurahia mwenzake, tuna uhusiano mzuri baina yetu. Siwezi kuwa mkimya katika hili zaidi ya kusema ukweli kuhusu matamanio yangu ya kufanya kazi na mtu huyu katika siku za maisha yangu ya soka.”

Wawili hao waliwahi kufanya kazi wakiwa Chelsea kuanzia mwaka 2013-2015, kabla ya Mourinho kutimuliwa na uongozi wa klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London, kufuatia matokeo mabovu yaliyomuandama msimu wa 2014/15.

Kwa kudhihirisha Willian haondoki Chelsea katika kipindi hiki, tayari uongozi wa klabu hiyo umeshakataa ofa ya Pauni milioni 37.7 iliyotumwa na mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona mwezi uliopita.

Mateo Kovacic atikisa kibiriti Real Madrid
'Kiki' yawaponza Roma na Stamina, Basata yakomaa nao