Mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona wapo tayari kufanya biashara na klabu ya Chelsea ya England, kwa kubadilishana wachezaji kutoka Brazil.

FC Barcelona wamefungua mjadala huo wakiamini huenda wakapata nafasi ya kuzungumza na uongozi wa Chelsea ili kuangalia uwezekano wa kumsajili kiungo mshambuliaji Willian Borges da Silva, ambaye ameonyesha kumpendeza meneja wao Ernesto Valverde.

Mabingwa hao wa Hispania, wamesema wapo tayari kumtoa kiungo wao kutoka Brazil José Paulo Bezerra Maciel Júnior (Paulinho), ambaye wanaamini atakua mbadala mzuri wa Willian endapo Chelsea wataafiki dili hilo.

Barcelona wamekuja na mbinu hiyo, baada ya ofa yao ya Pauni milioni 50 kukataliwa na uongozi wa Chelsea, huku wakisisitiza kulipwa Pauni milioni 70 ambazo ni sawa na Euro milioni 80.

Hata hivyo taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mundo Deportivo zimeleza kuwa, FC Barcelona wapo tayari kumjumuisha Paulinho katika dili hilo, sambamba na kutoa kiasi cha fedha ambazo hazikuwekwa wazi.

Wakati huo huo uongozi wa FC Barcelona huenda ukawapa nafasi nyingine Chelsea endapo watahitaji kuongeza mchezaji mwingine kutoka kwao, ili ajumuishwe kwenye dili hilo.

Wachezaji wanaotajwa kwa sasa ni Andre Gomes na Rafinha.

Mtibwa Sugar kushiriki kombe la shirikisho kwa masharti
Msigwa: Sifikirii kuwa Rais, lakini 2020 Chadema tunachukua nchi