Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara unaofadhiliwa UNDP imesema itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha uwiano wa kijinsia katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Violeth Mlinga ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua Warsha ya Wadau kuhusu ushiriki wa Kijinsia katika kupambana na ujangili huku akibainisha kuwa, “hatua hii inakuja kufuatia shughuli za uhifadhi kwa kiasi kikubwa kutawaliwa na uwakilishi wa wanaume na kuwepo kwa mitazamo kuwa kazi za uhifadhi zinawafaa zaidi wanaume kuliko wanawake.

Amesema, tathmini ya maandalizi ya mradi huo ilibaini kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia, licha ya kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika shughuli za uhifadhi na ili kuleta mapinduzi ya kifikra, Wizara na UNDP zinatoa uzito wa mapambano ya ujangili na biashara haramu ya nyara.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Bi.Violeth Mlinga ( katikati) akiwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori  Elisante Ombeni pamoja na Mkurugenzi  Mratibu wa Sera na Miradi wa UNDP, Amon Manyama,Kabla ufunguzi wa  Warsha ya Wadau kuhusu ushiriki wa Kijinsia  katika utekelezaji wa kazi za Uhifadhi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wanyamapori, Elisante Ombeni amesema suala la usawa wa kijinsia ni miongoni mwa masuala yanayotekelezwa kupitia kwenye Mradi huo ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa wingi zaidi katika uhifadhi

Naye, Mkurugenzi Mratibu wa Sera na Miradi wa UNDP, Amon Manyama, amesema ili kuleta matokeo chanya katika uhifadhi ni lazima kuboresha usawa wa kijinsia kwenye shughuli za kupambana na ujangili.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Violeth Mlinga (walioketi katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na mara baada ya kufungua Warsha ya Wadau kuhusu ushiriki wa Kijinsia katika utekelezaji wa kazi za Uhifadhi.

Amesema endapo Tanzania itafanikiwa kuleta usawa huo wa kijinsia itaweza kufikia lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu “2030 Agenda for Sustainable Development” linalohimiza kuwa usawa wa kijinsia ni muhimu kwa ulimwengu wenye amani, ustawi na uendelevu.

Warsha hiyo, imehudhuriwa na Maafisa Waandamizi kutoka UNDP, Wawakilishi kutoka WWF, WCS, AWF, PAMS Foundation pamoja na Wawakilishi wa Makamishna wa Uhifadhi kutoka TANAPA, NCAA, TAWIRI, TAWA.

Mwamuzi atumia Simu kama VAR Misri
Sadio Kanoute aahidi makubwa Simba SC