Uongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekivunja kitengo cha ujenzi ili kukisuka upya na kuweza kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Abel Makubi amesema maamuzi hayo yamekuja kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya ukaguzi wa jengo la hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi mwishoni mwa mwezi Agost mwaka huu.

“Tumekivunja kitengo hicho na kuleta watu wapya ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya wizara husuan ile ya ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa ambapo ujenzi wake umekua ukisuasua na hivyo kutokamilika kwa wakati. Prof. Makubi amesema kuwa wameshafanya tathimini ya miradi yote ya wizara ambayo imekua ikiendelea nchi nzima na kuona imekuwa ikichukua muda mrefu kutokamilika hilo ndilo lililafanya kukisuka upya kitengo hicho.

Amesema wizara yake haiwezi kuvumilia tena kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo kuwataka wale wote watakaoletwa wizarani hapo kutambua miradi yote inakamilika kwa wakati na lazima thamani ya fedha ionekane.

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa mnamo tarehe 27 Agosti mwaka huu alifanya ziara na kukagua ujenzi wa hospitali hiyo na kuagiza Wizara ya Afya kurejesha usimamizi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa ofisi ya Mkoa , ambapo wizara ya afya tayari imeshatekeleza agizo hilo kwa kuzirejesha hospitali zote za rufaa za mikoa kwenye usimamizi wa Makatibu Tawala wa Mikoa.

Rais Samia apewa jina jipya na Machifu
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 8, 2021