Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia , na Watoto, imepokea msaada wa vifaa vya upasuaji wa ugonjwa wa Ngiri, vitakavyotumika katika Hospitali ya Kivunge na Chakechake Pemba.

Akizungumza (kwa njia ya mtandao) katika halfa ya kukabidhi vifaa hivyo Wizarani hapo, Balozi wa China aliopo Zanzibar, Zhang Zhisheng amesema msaada huo wa vifaa tiba, umetolewa kwa lengo la kuwatibu wananchi wenye tatizo la Ngiri.

Ameleza kuwa, wagonjwa wasiopungua mia moja (100) watanufaika na msaada huo ili kuimarisha afya zao, na kuhakikisha tatizo hilo linaondoka nchini.

Balozi Zhang, amesema Serikali ya watu wa China inaendelea kuisaidia Zanzibar, hasa katika sekta ya afya na kuahidi kuendeleza ushirikiano ili kuisaidia serikali katika kuimarisha afya za wananchi wote.

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee , Jinsia na Watoto, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Abdulla Suleiman Ali, amesema msaada huo utaweza kuwasaidia wagonjwa wasiopungua mia nne, jambo ambalo litapelekea kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa jamii.

Amesema kuwa, misaada mingi inayotolewa na serikali ya China ikiwemo timu za madaktari, vifaa tiba pamoja na dawa ni jambo adimu ambalo lina umuhimu mkubwa  katika kuendeleza na kuimarisha huduma za afya nchini.

Sambamba na hayo Dk. Abdulla aliupongeza Ubalozi wa china kwa msaada huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano baina ya China na Zanzibar kwa maendeleo ya sekta ya afya.

Uchunguzi wabaini Hamza Gaidi
Waziri Mkenda atoa wito kwa vyama vya ushirika