Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewashukuru waganga wa tiba asili na tiba mbadala kwa ushirikiano katika afya za binadamu kwa ujumla huku serikali ikiendelea kutambua umuhimu wao.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa kamati kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Hanifa Selengu iliyofika mkoani Njombe kwa lengo la kuunganisha nguvu na Serikali ya Mkoa katika kupata namna bora ya kukomesha mauaji ya watoto yanayotokea mkoani Njombe.

“lengo la safari yetu ni kuja kuungana na kushirikiana na wataalamu wa mkoa wa Njombe ni kwa ajili ya kuangalia namna ya kuzuia au kuondokana na matatizo haya yanayojitokeza ya ukatili kwa kwa watoto, tumesikia mauaji yamejitokeza kwa mfululizo kwa hiyo kwa niaba ya katibu mkuu amenituma nitoe tamko la wizara kwa upande wa waganga wa jadi, anatoa wito kushirikiana katika kuwafichua waganga wenye kutoa masharti mabaya,”amesema Selengu

Aidha wizara hiyo imeomba vitendo vyote viovu na mifarakano miongoni mwa jamii vifichuliwe na kuchukuliwa hatua stahiki kwa wakati kutokana kuwepo njia mbali mbali za kufichua vitendo hivyo ikiwemo mamlaka za serikali za mitaa pamoja na jeshi la polisi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amewataka waganga hao wa tiba asili na tiba mbadala wa halmashauri ya mji wa Njombe na wengine mkoani humo kufanya kazi kutokana na utaratibu waliopewa huku akiagiza kuondolewa kwa mabango yanayotangaza uganga bila utaratibu maalumu.

Akizungumza kwa niaba ya waganga wa tiba asili Mganga Mpapai ameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na wataalamu hao huku akiomba kuendelea kupewa semina ya mara kwa mara ili kukumbushana.

Hata hivyo, Mwanasheria kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Denis Bashaka amesisitiza suala la kujikita katika kufichua tatizo linalosababisha kutokea kwa mauaji hayo na kuangalia namna bora ya kuzifikia jamii kutoa elimu na kuzingatia Sheria, Sera na Miongozo katika kuandaa jumbe zitakazoweza kutoa elimu.

 

Sababu yatajwa wanaume wenye umri mdogo kutunga mimba haraka wanawake wenye umri mkubwa
Mtoto aliyekatwa Koromeo mkoani Njombe afariki Dunia