Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja ikiwa na lengo la kuondoa kero za wananchi katika masuala ya ardhi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho leo Januari 7, 2022 Waziri wa Ardhi William Lukuvi alisema, kwa kutumia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na habari yaliyopo sasa wizara yake imeona zipo baadhi ya huduma za ardhi zinazoweza kutolewa kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii ambazo hazimlazimu mwananchi kufika ofisi za ardhi kitu ambacho kitasaidia kutoa huduma kwa haraka zaidi.

‘’Wizara imeanzisha kituo cha Mawasiliano kwa Wateja kitakachotoa huduma ya mawasiliano moja kwa moja na mwananchi kwa kutumia simu na ujumbe wa maneno kupitia Whatsup ambapo majibu au ufafanuzi utatolewa kwa wananchi na wataalamu wa ardhi,”Amesema Waziri Lukuvi.

Aioidha Kituo hicho cha Mawasiliano kwa Wateja kina wataalamu wabobezi katika masuala ya ardhi waliopata mafunzo yakinifu ya kuifanya kazi ya kutoa huduma kwa wateja kwa weledi na kutoa majibu kwa wakati.

Kupitia kituo hicho mwananchi atalazimika kupiga simu na kuongea moja kwa moja na watoa huduma kupitia namba 0739-646-885 au kutuma ujumbe wa maneno kupitia mtandao wa WhatsApp kwa namba hizo. Kituo hicho kitakuwa wazi siku za kazi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Sambamba na hayo yote Waziri Lukuvi ametoa rai kwa wananchi kukitumia kituo hicho kwa kupiga simu na kutuma ujumbe wa maneno kupitia namba ya simu iliyotangazwa na kutumia tovuti ya wizara kupata huduma kwa urahisi bila usumbufu ili kuepuka gharama za kusafiri sambamba na kutumia muda mwingi kufuata huduma hizo ofisi za wizara makao makuu, ofisi za ardhi za mikoa na halmashauri.

Madini yailipa Serikali kupita kiwango
Fraga awekewa ngumu kujiunga Simba SC