Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imevuka lengo la kukusanya kodi kwa zaidi ya asilimia 100 kwa kukusanya Tsh. Bilioni 74.098. kati ya Julai 1, 2015 hadi June 30, 2016.

Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Kodi katika Wizara hiyo, Bw. Dennis Masami wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Saba Saba.

“Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya Tsh. bilioni 70 na hadi kufikia Juni 30, 2016 kiasi cha Tsh. 74,098,902,895.20/= kimekusanywa sawa na asilimia 106 ya zaidi ya lengo,”alisema Masami.

Masami amesema kwamba ukusanyaji huu wa ufanisi umetokana na elimu iliyotolewa na Wizara kwa walipa kodi na kuwaandikia hati za madai wadaiwa sugu ambao walikuwa hawalipi kodi kwa wakati.

Kwa mujibu wa Masami mashauri 5000 yamefunguliwa  ambapo Wizara imeshinda mashauri 2000 na imepewa hati ya kukamata mali ambayo ni deni la zaidi ya Tsh. bilioni 6 kati ya hizo zaidi ya bilioni 3 zimelipwa na wadeni wengine wanaendelea kulipa.

Aidha, amewataka wamiliki wote wa ardhi kulipa kodi kwa wakati na kwamba kodi ya ardhi hulipwa kila ifikapo Julai 1 ya kila mwaka katika Halmashauri, Manispaa na Makao Makuu ya Wizara na kuongeza kuwa kulipa kodi ni wajibu wa kila mmiliki kwa mujibu wa kifungu cha 33(1) cha sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999.

“Kwa watakao kaidi kutimiza masharti hayo watachukuliwa hatua za kisheria chini ya fungu la 50 sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999; pamoja na kuwafikisha mahakamani, kukamata mali ili kufidia deni au kufuta milki,”alisema Masami

CAF Yaipeleka Tanzania Ufukwe Wa Pwani Ya Afrika Ya Magharibi
Video: Waziri wa Israel azuru Uganda