Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inakusudia kuandaa Sera Mpya ya Sanaa kwa lengo la kuunda sheria itakayosimamia maslahi ya wasanii nchini.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye alipokuwa akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC 1).

“Sera ya Utamaduni iliyopo sasa ina mapungufu  kwani haijaeleza vizuri namna inavyowanufaisha wasanii na kusimamia kazi zao ‘’  Alisema Mhe. Nape.

Aliongeza kuwa wizara inaendelea na mchakato wa kuandaa Sera ya Sanaa ambayo itakuwa suluhisho katika uundaji wa sheria nzuri itakayosimamia kazi za wasanii na kubainisha kuwa mchakato huo utawashirikisha wadau mbalmbali.

Aidha Mhe. Nape alieleza kuwa serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wasanii katika uendeshaji wa biashara zao,  hasa kipato kidogo kisichoendana na kazi zao, kazi zao kuingiliwa na watu wasiohusika ambao wamekuwa wakijinufaisha wenyewe na uuzwaji  holela wa kazi za wasanii kutoka nje nchini.

Hata hivyo katika kudhibiti vitendo hivyo wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imekuwa ikiendesha msako katika maeneo mbalimbali ili kuwabaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria wale wote wanaohujumu kazi za wasanii hapa nchini.

Kuhusu Sekta ya Utamaduni alisema kuwa watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kujituma na kuacha tamaduni ambazo ni kinyume na  maadili ya mtanzania hasa vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike, ndoa za utotoni na baadhi ya wazazi kutosomesha watoto wa kike.

Mh. Nape alitoa wito kwa wataalam wa lugha ya Kiswahili kuandika vitabu vingi zaidi vitakavyosaidia kuikuza lugha hiyo pia wasanii  kwenda katika vyuo vya sanaa kupata utaalam utakaowawezesha kufanya kazi zao katika ubora na mvuto zaidi

Sheria Ya Kuwalinda Watoa Taarifa Za Uhalifu Na Mashahidi Yaanza Kutumika
Ukweli Wa Mrisho Ngassa Kusajiliwa Mbeya City FC