Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema kuwa ipo haja ya kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazamkabili mkulima na Sekta hiyo kwa ujumla.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa kikao cha siku mbili baina yake na Watafiti wa kilimo kutoka Taasisi mbalimbali za kilimo nchini.

Amesema kuwa Sheria zinazotumika kwa sasa ni za Bodi za Mazao mbalimbali, ambazo pia zinachangamoto zake na kuna mazao ambayo hayana Bodi kiasi kwamba kuwatetea Wakulima wa mazao hayo inakuwa vigumu.

“Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo, kwa sababu hatuna Sheria ya Kilimo na inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo, iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya” amesema

Aidha, mazao yaliyopo katika utaratibu wa Bodi ni pamoja na zao la Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Pareto na Tumbaku kwa upande wa mazao ya biashara, mazao ambayo hayana bodi ni yale ya chakula ambayo nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

Waziri Hasunga amewataka Watafiti hao kutumia kikao hicho kutoa michango yenye tija, nini kifanyike katika Sekta ya Kilimo kwakuwa Watafiti wana wigo mpana wa kuitoa Sekta hiyo kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema kuwa kikao hicho ni cha kipekee kwakuwa kimewakutanisha Watafiti na Wataalamu kutoka Taasisi za utafiti na watafiti wakufunzi wabobevu kutoka vyuo vya kilimo nchini.

Naye mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele Dkt. Fortunus Kapinga amesema kikao hicho kimekuja wakati muafaka ambapo utafiti wenye tija na wenye kuzingatia wakati unahitajika zaidi ili kutatua changamoto za kilimo nchini.

Maelfu ya raia waandamana nchini Italy
Mswada wa sheria ya vyama vya siasa wawakosha wabunge CCM