Shirikisho la soka nchini TFF, limetoa shukurani kwa wanafamilia ya soka waliotuma salamu za rambirambi kutokana na msiba wa Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh Said Muhammad aliyefariki dunia Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na TFF imeeleza kuwa, hayati Sheikh Said Muhammad alikuwa hazina katika soka la Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mchango ya mawazo na miongozo katika Kamati ya Utendaji ya TFF.

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Muhammad aliongoza Klabu ya Azam FC kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe.

Kutokana na kufariki kwa Sheikh Muhammed, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amempendekeza Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Yahya Hamad – kukaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji Ligi (Kamati ya Saa 72) ili kushughulia masuala yote ya mechi zilizochezwa tangu mwanzo wa Novemba, 2016 baada ya kifo cha Sheikh Muhammad.

“Tunachukua nafasi hii kutoa wito kwa klabu kumpa ushirikiano Bwana Hamad katika majukumu yake mapya akiongoza kamati hiyo yenye wajumbe ambao ni Baruan Muhuza (Azam Tv), Boniface Wambura (Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi), Jonas Kiwia (Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano TFF), Philemon Ntahilaja (Mdau wa Mpira wa Miguu), Charles Ndagala (Katibu Kamati ya Waamuzi ya TFF), Kanali Mstaafu wa JWTZ, Isaron Chacha na Steven Mnguto ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya ligi.” Imeeleza taarifa ya TFF

Kumekucha Azam Sports Federation Cup
Video: Ommy Dimpoz amkejeli Nay wa Mitego kwa majanga yaliyompata