Mshambuliaji kutoka nchini Argentina Jonathan Calleri amekamilisha taratibu wa kujiunga na wagonga nyundo wa jijini London (West Ham Utd), akitokea kwenye klabu ya Deportivo Maldonado ya Uruguay.

Calleri anakuwa mchezaji wa sita kutoka nchini Argentina kusajiliwa na klabu ya West Ham Utd baada ya kutanguliwa na Lionel Scaloni, Javier Mascherano, Carlos Tevez, Mauro Zarate pamoja na Manuel Lanzini ambaye bado yupo kikosini kwa sasa.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, jana alianza mazoezi rasmi sambamba na wachezaji wenzake wa West Ham Utd huko Rush Green na huenda kesho akawa sehemu ya kikosi cha Slaven Bilic ambacho kitapambana na Astra Giurgiu katika mchezo wa mchujo wa michuano ya  Europa League.

“Ni ukarasa mwingine katika maisha yangu ya soka, sina budi kumshukuru mungu kwa hatua hii niyoipiga na nina hakika nitacheza soka kwa malengo zaidi tofauti na nilipokua.

“Nilicheza kwa kujituma wakati wote wakati nikiwa na Deportivo Maldonado na kufikia hatua ya kuonwa na West Ham Utd, na nina ahidi hapa nitacheza vizuri zaidi kwa kusaidiana na wenzangu ili kutimiza malengo yanayokusudiwa.

“Nimekua mchezaji ambaye nina uchu wa mafanikio, na jambo hilo siku zote limekua kama nguzo kwangu.” Alisema Jonathan Calleri dakika chache baada ya kusaini mkataba wa mkopo wa kuitumikia West Ham Utd.

Calleri mwenye umri wa miaka 22, ameondoka nchini Uruguay na kuacha kumbukumbu ya kufunga mabao 21 katika michezo 53 aliyoitumikia klabu ya Deportivo Maldonado. Alitengeneza nafasi za magoli kwa kupiga pasi 11 za mwisho katika michezo 53 ya klabu hiyo ambayo ilimsajili kwa mkopo akitokea nchini kwao alipokua mchezaji wa Boca Junior ambayo aliisaidia kutwaa ubingwa wa Primera Division pamoja na Copa Argentina mwaka 2015.

Everton Kufuta Ndoto Za Moussa Sissoko
Mourinho Aibuka Na Bishara Ya Kubadilishana Wachezaji