Aliyekuwa kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi leo amesaini Mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuwa Kocha Msaidizi wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo umempa mkataba wa mwaka mmoja na nusu na ataanza kibarua chake kesho.

Tiboroha amesema kwamba maamuzi ya kumchukua Mwambusi na kuachana na mapendekezo ya awali ya kuleta msaidizi kutoka nje ya nchi yanatokana na kocha huyo kuifahamu vizuri Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambayo Yanga ndiyo mabingwa watetezi.

“Tayari Mwambusi ni kocha wetu, nimeshamsainisha mkataba leo hii,” alisema Tiboroha.

Aliongeza kwamba wanaamini Mwambusi atakuwa na mchango mkubwa kwa timu hiyo ambayo mwakani itashiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame.

Mwambusi amewaachia simanzi viongozi wa Mbeya City, timu ambayo aliipandisha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013-2014 na kuwa tishio nchini ndani ya muda mfupi.

Lakini dau zuri ambalo Yanga SC wamempa mwalimu huyo wa zamani wa Moro United limemfanya akubali kuiacha timu ya mkoa wa nyumbani, ambayo hata yeye anaipenda.

Mwambusi anachukua nafasi ya Charles Boniface Mkwasa aliyekuwa Msaidizi wa Mholanzi, Hans van der Pluijm, ambaye amehamia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Magufuli Akabidhiwa 'Faili' La Wasaliti Awashughulikie
CCM Yaahidi Neema Mpya Kwa Wafanyabiashara Wadogo