Mabingwa wa Soka Tanzania bara Klabu ya Yanga, wamepoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ugenini dhidi ya U.S.M Alger kwa kuchezea kichapo cha mabao 4-0 na kushika mkia katika kundi D.

Mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo jijini Algiers, Yanga iliruhusu mabao mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya kuongezwa mengine mawili kipindi cha pili na kufanya waondoke bila alama huku wakiwa na deni kubwa la mabao ya kufungwa.

Aidha, katika Kundi D, Yanga inashika nafasi ya nne ambayo ni ya mwisho baada ya mechi nyingine ya kundi hilo iliyopigwa usiku huo huo kati ya wenyeji Rayon Sport ambao walitoka sare ya bao 1-1 na  Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.

Kwenye ligi kuu Tanzania Bara, Yanga inashika nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC ikiwa na alama 48 kwenye mechi 24 ilizocheza hadi sasa. Azam ina alama 49 kwenye mechi 27 na Simba ina pointi 65 baada ya mechi 27.

Hata hivyo, kundi D sasa linaongozwa na U.S.M Alger yenye alama 3 ikifuatiwa na Gor Mahia yenye alama 1 sawa na Rayon Sports yenye alama moja pia huku Yanga ikiwa haina alama baada ya kupoteza mechi yake.

 

Kocha wa zamani wa Yanga afariki dunia
Mfanyabiashara amdai Ali Kiba matunzo ya mtoto Mahakamani