Mchezo wa Ligi kuu Tanzania Bara kati Yanga na African Spots umemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 kwenye mchezo ulichezwa kwenye dimba la Taifa.

Yanga ilijipatia bao lake la kwanza kupitia kwa mlinzi wake wa kati, Kelvin Yondani kwenye dakika ya 32 ya mchezo.

Dakika tano baada ya bao la kwanza, mshambuliaji Donald Ngoma akiitumia kiustadi krosi ya Haruna Niyonzima aliyemtafuta akiwa ndani ya sita aliiandikia Yanga bao la pili murua kwenye mchezo huo.

Baada ya kurudi kutoka kwenye mapumziko, Yanga ilijihakikishia kuzinyakua pointi tatu kwenye mchezo huo baada ya Amissi Tambwe kuifungia bao la tatu timu yake kwenye dakika ya 52 ya mchezo huo.

Akitokea benchini, Matheo Anthony alizidi kushindilia msumari wa moto kwenye kikosi cha African Sports kwenye dakika ya 59 ya mchezo na kuifanya Yanga kuongoza kwa mabao 4-0.

Kama haitoshi mshambuliaji raia wa Burundi, Amissi Tambwe alifunga bao la pili kwa upande wake kwenye mchezo huo na la tano kwa Yanga iliyoonekana kuwa kwenye wakati mzuri zaidi kuliko African Sports.

Kwenye mchezo huo Yanga walionekana kuwa hatari zaidi kwani mpaka dakika ya saba ya mchezo huo, Yanga ilionyesha kuwa hatari zaidi ya African Sports.

Juma Abdul angeweza kuutumia vizuri mpira uliopigwa na kiungo wa timu yake ya Yanga, Thabani Kamusoko lakini mpira huo ulipaa juu kunako dakika ya 15 kwenye kipindi cha kwanza.

Mfungaji wa bao la pili la Yanga, Donald Ngoma alimpisha Matheo Anthony kwenye mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua.

African Sports walionekana kutokuwa na madhara langoni mwa Yanga baada ya mabingwa hao watetezi kuonekana wakicheza kama wapo mazoezini.

Kufuatia matokeo hayo, Yanga inapaa kileleni na kuwashusha mahasimu wao, Simba SC baada ya kufikisha pointi 50 huku Simba SC ikisalia na pointi zake 48 katika nafasi ya pili wakifuatiwa na Azam wenye pointi 47 katika nafasi ya tatu.

Mkurugenzi Wa Ufundi ZFA Atumbuliwa Jipu
Licha Ya Kuambulia Kisago Cha 2-1, Twiga Stars Wajazwa Noti