Kiungo wa Man City Yaya Toure amepingana na meneja wake Pep Guardiola kuhusu uwezekano wa klabu hiyo kuwa miongoni mwa watakaofanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi ya nchini England mwishoni mwa msimu huu.

Guardiola alitangaza kujiondoa katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu wa 2016/17, baada ya kupokea kisago cha mabao manne kwa sifuri mwishoni mwa juma lililiopita dhidi ya Everton.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania anaamini itakua ni sawa na ndoto za Alinacha kuifikia Chelsea iliyo kileleni mwa msimamo wa ligi ya England kwa tofauti ya point 10 dhidi ya kikosi chake.

Yaya Toure ameibuka na mtazamo tofauti kuhusu kauli ya bosi wake na kueleza kuwa, bado Man city wana nafasi ya kutosha ya kutwaa ubingwa na ni mapema mno kukata tamaa.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 amesema: “Nafikiri katika ligi ya nchini England (Premier League) kila kitu kinawezekana. Katika mchezo wa soka unatakiwa kuwa na mawazo chanya.

“Nafahamu ugumu na ushindani uliopo katika ligi hii, lakini hauwezi kujinasua katika fikra za kutwaa ubingwa kwa kigezo cha kikosi chako kupoteza mchezo mmoja ama miwili, kwangu mimi siafikiani na yoyote anaeiondoa Man city katika wimbi la ubingwa katika kipindi hiki.”

Kwa matokeo ya kufungwa mabao manne kwa sifuri, Man City iliporomoka hadi katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ya nchini England, huku ikiwa na point 42.

Dismas Ten: Maandalizi Yamekamilika
Hali Bado Ngumu Kwa Dimitri Payet